Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afya ya wahamiaji ni muhimu kufanikisha SDGs

Afya ya wahamiaji ni muhimu kufanikisha SDGs

Huko Colombo, Sri Lanka mashauriano ya siku mbili kuhusu afya ya wahamiaji yamehitimishwa kwa kupitishwa kwa tamko la Colombo linalotaka ushirikiano wa kimataifa ili kuboresha afya na ustawi wa wahamiaji na familia zao.

Ukiwa umeitishwa na shirika la la afya duniani, WHO na lile la wahamiaji, IOM kwa ushirikiano na serikali ya Sri Lanka, mkutano huo umebaini kuwa kulinda afya ya kundi hilo ambalo kila wakati liko kwenye kuhamahama, ni muhimu afya ya umma na haki ya kibinadamu.

Washiriki wamesema idadi ya wahamiaji ikiwa imefikia bilioni moja hivi sasa, mahitaji ya afya ni makubwa na mifumo ya afya inahaha kukidhi mahitaji yao, afya ambayo ni muhimu kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Msemaji wa IOM, Joel Millmana amesema tamko la Colombo linatoa wito wa kujumuisha afya ya wahamiaji kwenye ajenda ya kitaifa, kikanda na kimataifa na kuendeleza mshikamano wa kimataifa kwa sera sawia za afya ya wahamiaji na kuwa na ajenda ya pamoja na mifumo ya kimataifa inayohakikisha kuwa afya ya wahamiaji inalindwa.