Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa mawili, Israeli na Palestina ndio suluhu pekee Mashariki ya Kati: UM

Mataifa mawili, Israeli na Palestina ndio suluhu pekee Mashariki ya Kati: UM

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov amewaambia wanachama wa Baraza la Usalama hivi leo Alhamisi kuwa ufumbuzi wa mataifa mawili bado ndio njia pekee ya kufikia maazimio ya amani  kati ya Israeli na Wapalestina.

Bwana Mladenov ameonya kuwa misimamo mikali, kutovumiliana, vurugu na dini ni baadhi ya changamoto zinazoikabili eneo hilo akitaja kuwa inabidi pande zote mbili kupunguza matamshi yao yanayoweza kuzusha tafrani ingawa viongozi wanatambua ushirikiano kwa ajili ya usalama.

Akizungumza kwa njia ya video, mratibu huyo maalum ameonyesha wasiwasi wake juu ya tishio la kile alichokiita dimbwi la misimamo mikali ya kisiasa inayojitokeza kwenye kanda hiyo. Amesema ni muhimu kuelewa kwamba kamwe wasiruhusu mgogoro wa Israel na Palestina kuingia kwenye dimbwi hilo. Wapalestina, Israel na jumuiya ya kimataifa lazima kuwajibika ili kuepuka kuenea kwa mvutano.

Pia ametoa wito wa kujiepusha kuchukua hatua za moja moja ambazo zinaweza kuzusha mapambano. Mladenov amekosoa upitishwaji wa sheria ya ujenzi holela wa makazi ya walowezi katika ukingo wa Magharibi kwenye ardhi inayomilikiwa na Palestina akionya kuwa sheria hizo zinaweza kuleta madhara kwa Israel na kuzorotesha ufumbuzi wa mataifa mawili.

(SAUTI YA MLADENOV)

Kuendelea kwa hali mbaya ya usalama Gaza imeongezeka zaidi kwa upande wa misaada ya kibinadamu na maendeleo kwa sababu ya kufungwa kwa mipaka kati yao na mgawanyiko wa kisiasa. Msimu huu wa baridi umeleta changamoto nyingi kwa upande wa umeme ambapo raia wa Gaza mwezi Desemba walijikuta katika saa mbili pekee za kupata umeme kwa siku, mamia kwa maelfu ya watu walifanya maandamano kupinga na wengi wao kuzuiliwa ikiwemo waandishi wa habari. Kwa ukarimu wa mchango wa serikali ya Qatar wa dola milioni 12. Umoja wa Mataifa na wadau wengine wanashughulikia njia endelevu ya kutatua swala hilo la umeme.