WFP kuendelea kutoa msaada wa chakula mashariki mwa Ukraine

15 Februari 2017

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP litaendelea kusaidia watu 220,000 wenye uhaba wa chakula katika maeneo ya misukosuko ya vita mashariki mwa Ukraine katika kipindi cha 2017, na kuongeza juhudi kuwasaidia kujiwezesha.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo wastani watu milioni 3.1 wana haja ya msaada wa kibinadamu, na jamii nchini Ukraine wakiwa wanaendelea kushuhudia madhila ya mgogoro wa miaka mitatu.

Mwakilishi wa WFP nchini Ukraine Dorte Ellehammer amesema kuwa hali inazidi kuwa mbaya zaidi na bei ya vyakula kuongezeka kwa kasi kabisa ikilinganishwa na mapato, ukosefu wa ajira na uwezo wa familia kujimudu kwa chakula wanachohitaji, jamii nyingi sasa zinategemea mikakati mbadala kukabiliana na matatizo ya kiuchumi.

Mwaka huu WFP itaendelea kutoa msaada wa chakula kwa watu 70,000 wanaoishi katika mazingira magumu na itawalenga wazee, familia zinazoongozwa na mama pekee, watu wenye magonjwa sugu au ulemavu, pamoja na wale ambao hawapati misaada ya kibinadamu ya aina yoyote.

WFP imesema kuwa watu 150,000 wenye matatizo ya kupata au kununua chakula cha kutosha kila siku watashirikishwa katika mpango wa mafunzo kwa chakula na shughuli za biashara.

Tangu Novemba 2014, WFP imetoa msaada wa chakula wa dharura kwa wakimbizi wa ndani na wale wanaorejea kwa wakazi mashariki mwa Ukraine takriban 850,000 licha ya mgogoro unaoendelea na hali tete ya usalama.