Hakuna masomo ya wavulana au wasichana pekee- Katherine
Leo ni siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana kwenye sayansi ambapo Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO linapigia chepuo uhamasishaji wa makundi hayo kushiriki katika fani hiyo.
Uhamasishaji huo unazingatia fikra potofu katika baadhi ya jamii kuwa masomo ya sayansi, hisabati na uhandisi ni kwa ajili ya wanaume na wavulana huku wasichana na wanawake wakionekana kuwa na uwezo wa sayansi za jamii pekee.
Akitoa ujumbe wake kwa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesihi jamii ya kimataifa kuazimia kutokomeza upendeleo, kuhakikisha uwekezaji zaidi kwenye elimu ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati kwa wanawake na wasichana kote duniani, halikadhalika fursa kwa ajira zao.
Katika video hii ni msichana Katherine Jin mwanasaynsi aliyeweza kuvuka viunzi vya fikra potofu na anasimulia jinsi ugunduzi wake wa kisayansi unavyosaidia kulinda afya za wahudumu wa afya.