Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres asikitishwa na hatua ya Israel kwa wapalestina

Guterres asikitishwa na hatua ya Israel kwa wapalestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres ameelezea kusikitishwa kwake ni kitendo cha bunge la Israel, kupitisha muswada wa sheria unaowezesha Israel kutumia ardhi ya wapalestina kwa ujenzi wa makazi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu New York, Marekani hii leo, amemnukuu Guterres akisema kuwa hatua hiyo ya Jumatatu ni kinyume na sheria za kimataifa na itakuwa na athari za kisheria kwa Israel.

Yaelezwa kuwa sheria hiyo inaweka kinga dhidi ya makazi ya walowezi wa Israel huko ukingo wa magharibi wa mto Jordan, licha ya kwamba maeneo hayo ni ya wapalestina.

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu anasisitiza umuhimu wa kuepuka hatua zozote zinazoweka kupeleka mrama hoja ya uwepo wa mataifa mawili. Masuala yote ya msingi yanapaswa kusuluhishwa kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya pande mbili hizo kwa msingi wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwa makubaliano kati ya pande mbili.”

Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kuendelea usaidia mchakato huo.