Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNOCHA yasaka dola milioni 864 kukwamua wananchi wa Somalia

UNOCHA yasaka dola milioni 864 kukwamua wananchi wa Somalia

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, UNOCHA, imezindua ombi la dola milioni 864 kwa ajili ya kushughulikia mahitaji ya kibinadamu nchini Somalia kwa mwaka huu wa 2017.

Uzinduzi huo umefanyika kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu ukilenga kukwamua watu milioni 3.9 nchini humo wanaohitaji msaada wa dharura wa chakula.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Naibu mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Peter de Clercq amesema..

(Sauti ya de Clercq) 

“Kwa hiyo basi nasisitiza wito wangu kwa jamii ya kimataifa kuimarisha usaidizi wazo kwa wananchi wa Somalia. Fedha hizi zikipatikana zitaendelea kuokoa maisha na kuimarisha mbinu za kuishi, kwani zitawapatia huduma za msingi na kuwaepusha watu walio hatarini zaidi.”

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na spika wa bunge la Somalia, Mohamed Sheikh Osman Jawari, maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa na wale wa kibalozi nchini Somalia.

Ombi hilo limetolewa wakati huu ambapo Somalia inakabiliwa na ukame mkubwa uliosababisha watu milioni tano sawa na asilimia 40 ya wananchi wa Somalia kukabiliwa na uhaba wa chakula.