Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zinaendelea kupeleka kikosi cha kikanda Sudan Kusini

Juhudi zinaendelea kupeleka kikosi cha kikanda Sudan Kusini

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS imetoa taarifa za kukanusha ripoti kwenye vyombo vya habari kuhusu kupelekwa kwa kikosi cha ulinzi cha kikanda nchini humo.

UNMISS bila ya kutaja madai inayokanusha, imesisitiza kuwa katika maandalizi ya kuwasili kwa kikosi hicho, inaendelea na mashauriano na serikali ya mpito ya Umoja wa Kitaifa h uko Sudan Kusini.

Mathalani UNMISS imesema wanajadili kuhusu ni eneo gani askari wa kikosi hicho watapelekwa kwenye mji mkuu Juba.

Taarifa hiyo imekumbusha kuwa Baraza la Usalama kupitia azimio 2304 liliamua kuongezwa kwa askari kufikia 17,000, ikiwemo askari 4,000 wa kikosi hicho cha kikanda.

Halikadhalika imesema serikali ya Umoja wa Kitaifa iliridhia kupelekwa kwa kikosi hicho bila masharti yoyote kupitia taarifa yake kwa Baraza la Usalama tarehe 30 mwezi Novemba mwaka jana.