Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame kuongeza makali ya njaa pembe ya Afrika- FAO

Ukame kuongeza makali ya njaa pembe ya Afrika- FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema nchi za pembe ya Afrika zinaweza kushuhudia ongezeko la njaa kwa kuwa jamii zinaendelea kukabiliana na mchanganyiko wa madhara ya ukame uliokumba ukanda huo mwaka huu.

FAO imesema hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa kuwa idadi ya wakimbizi inaongezeka kwenye eneo hilo na hivyo kuongeza makali ya ukosefu wa uhakika wa chakula na lishe bora.

Kwa sasa watu milioni 12 huko Ethiopia, Kenya na Somalia wanahitaji msaada wa chakula kutokana na kuporomoka kwa uzalishaji kwenye sekta ya kilimo, mifugo na akiba ya mbegu.

Mathalani ukame umesababisha wafugaji kuuza mifugo yao kwa bei ya chini na hivyo kuongeza makali zaidi.

Skukri Ahmed, ni mchumi mwandamizi wa FAO kwenye pembe ya Afrika.

(Sauti ya Skukri)

“Tayari tumeanza usaidizi kwa wakulima kabla ukame haujapiga. Na pia kwa wafugaji tunanunua mifugo kabla haijapungua uzito, hivyo tunasogeza soko karibu na wafugaji. Halikadhalika tunawaletea chakula cha mifugo na kukiweka maeneo muhimu ili wafugaji watumie kuokoa mifugo yao.”