Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulaya yafungiwa milango Afrika Magharibi

Ulaya yafungiwa milango Afrika Magharibi

Mataifa matano ya Afrika Magharibi yamepiga marufuku uingizaji wa mafuta yenye kiwango cha juu cha salfa kutoka Ulaya na hivyo kusaidia watu zaidi ya milioni 250 kuvuta hewa safi na salama.

Nigeria, Benin, Ghana, Togo na Cote d’Ivoire zimechukua hatua hiyo ambapo shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP limesema itapunguza kwa kiasi kikubwa hewa chafuzi kutoka kwenye magari .

Mataifa hayo yameweka sheria kali za kutumia dizeli yenye kiwango kidogo cha Salfa, halikadhalika viwango vya utoaji hewa chafuzi kwenye magari, hatua inayofunga soko la mafuta machafu ya Ulaya huko Afrika Magharibi.

Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Erik Solheim amesema Afrika Magharibi inatuma ujumbe thabiti kuwa haikubali tena mafuta machafu toka Ulaya na ni kiashiria kuwa wanaweka mbele afya ya umma.

Mafuta kutoka Ulaya yaliyokuwa yakiuzwa Afrika Magharibi yana kiwango cha Salfa mara 300 kuliko kiwango kinachoruhusiwa Ulaya.