Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa ECCAS wapazia sauti makubaliano DRC

Viongozi wa ECCAS wapazia sauti makubaliano DRC

Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya uchumi kwa nchi za Afrika ya Kati, ECCAS, wametoa wito kwa pande za kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambazo hazijajiunga na mkataba wa amani uliotiwa saini tarehe 18 mwezi Oktoba kufanya hivyo mara moja.

Wamesema hayo katika taarifa yao ya pamoja mwishoni mwa mkutano wao huko Libreville, Gabon ulioangazia masuala ya ugaidi na amani ukanda wa Afrika ya Kati, wakiongeza kuwa pande ambazo zimesaini, zizingatie makubaliano hayo.

Wametoa wito kwa pande za kisiasa na kijamii kujumuika kwenye mkataba huo ili kuimarisha utangamano wa kijamii na maandalizi salama ya uchaguzi wa kidemokrasia uliopangwa kufanyika mwezi Aprili mwaka 2018.

Miongoni mwa marais walioshiriki ni Ali Bongo Ondibmba wa Gabon, Idriss Deby wa Chad, Paul Kagame wa Rwanda, Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati huko Joseph Kabila wa DRC akiwakilishwa na waziri wake wa mambo ya kigeni, Raymond Tshibanda.