Skip to main content

Watu 400,000 wahitaji malazi Aleppo

Watu 400,000 wahitaji malazi Aleppo

Umoja wa Mataifa umesema takribani watu 30,000 waliokimbia mapigano huko Aleppo nchini Syria wanapata misaada ya kibinadamu lakini mamia ya maelfu  wanahitaji msaada zaidi ikiwemo malazi.

Mjumbe maalum wa umoja huo kuhusu Syria Staffan de Mistura amesema hayo leo huko Geneva, Uswisi akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kikao cha kikosi kazi cha kikundi cha usaidizi cha kimaitafa.

Ametaja kuwa huko Aleppo, Mashariki watoa huduma za misaada bado wanashindwa kuwafikia wahitaji walio maeneo ya  upinzani.

(Sauti ya de Mistura)

 “Hii leo mjini Aleppo kuna wakimbizi wa ndani 400,000, hebu fikiria, kimsingi ni sawa na idadi ya wakimbizi wote wa Syria walioko Ulaya.”

Amesema kwa sasa Umoja wa Mataifa unatuma timu maalum kuingia Aleppo kusaidia usambazaji wa misaada na pia kuhakikisha waliokimbia makazi hawakumbwi na zahma.

Hapo jana mkuu wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa alionya kuwa Aleppo iko hatarini kuwa kaburi moja la wengi.