Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunasikitishwa na uamuzi wa Kenya kuondoa vikosi Sudan Kusini - Ladsous

Tunasikitishwa na uamuzi wa Kenya kuondoa vikosi Sudan Kusini - Ladsous

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa usalama kwenye Umoja wa Mataifa Hervé  Ladsous amesema wamesikitshwa na uamuzi wa Kenya kuondoa vikosi vyake vya kulinda amani Sudan Kusini, sanjari na mchakato wa amani nchini humo.

Amesema hayo akijibu maswali ya wanahabari jijini New York, Marekani baada ya Kenya kupitia mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Macharia Kamau kutangaza hatua hiyo kufuatia kuondolewa kwenye nafasi ya ukamanda wa vikosi vya Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini, UNMISS Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki.

(Sauti ya Ladsous)

“Ni uamuzi wa taifa hilo, tunaheshimu, lakini nasikitika. Tunatathmini athari yake kwenye kikosi cha kikanda kilichoidhinishwa hivi karibuni na Baraza la Usalama. Tunajaribu kulitekeleza haraka iwezekanavyo.”

image
Mwakilishi wa kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Macharia Kamau. (Picha:UN/Evan Schneider)
Awali Balozi Macharia alielezea msingi wa uamuzi wao ambapo amesema ingawa vitendo vilivyofanyika mwezi Julai si sahihi na hawavitetei...

(Sauti ya Balozi Kamau)

“Haiwezi kuwa sahihi kwamba mtu mmoja tu abebe mzigo wa kushindwa kwa mfumo mzima, kama ilivyo kisa cha tukio hili. Uchunguzi usingalielekezwa kwa Kamanda wa vikosi pekee, ambaye alikuwa na wiki tatu tu, visa hivi vilipotokea. Badala yake ungalijika kwenye mfumo mzima ikiwemo umuhimu wa uwajibikaji kuanzia Idara ya ulinzi wa amani hapa makao makuu hadi kamandi ya pamoja UNMISS Juba.”

Uchunguzi huru ulioitishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ulibaini kuwa UNMISS haikuwa na mwongozo wa kutosha wakati wa ghasia za mwezi Julai mwaka huu huko Juba ambako watu 73 waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa