Skip to main content

Hatutokata tamaa kufikisha misaada Aleppo: Egeland

Hatutokata tamaa kufikisha misaada Aleppo: Egeland

“Hatukati tamaa, kuwahamisha wagonjwa na majeruhi Mashariki mwa Aleppo, amesema leo mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya Syria.

Jan Egeland amejutia kushindwa kwa mpango wa Umoja wa mataifa kuhamisha watu wiki iliyopita, na kudai kwamba pande hasimu kwenye maeneo yanayozingirwa ya Aleppo , waondoe vikwazo ili kuruhusu misaada zaidi kuingia.

Bwana Egeland amesema hakuna chakula au madawa yaliyoruhusiwa kuingia Aleppo kwa miezi mine na Umoja wa Mataifa una mipango mitatu ya muda mrefu ya kupeleka misaada na utaendelea kufuatilia hilo.

Ameongeza kuwa mosi, takribani watu 1,000 wagonjwa na majeruhi pamoja na familia zao wanahitaji kuhamishwa kwa ajili ya kupatia matibabu haraka.

Pili vifaa na dawa kwa ajili ya matibabu vinahitajika haraka, kwa ajili ya kutibu raia waliokwama kwenye maeneo hayo, na mwisho Umoja wa Mataifa ulipanga kutumia usitishaji uhasama wa wiki iliyopita kuingiza misaada ya chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu. Lakini pande hasimu zikaweka maslahi yao mbele akiongeza

(SAUTI YA EGELAND)

“Sote tumefeli, hakukuwa hata na mpango mmoja wa kuhamisha watu ulioandaliwa, au hata lori moja lililoingia na misaada. Hivyo ni funzo na mchakato unaendelea kwa sababu hatukati tamaa.Tunaanza tena leo kujaribu kufanya mambo hayo matatu.”

Amesema licha ya ushirikiano wa Marekani na Urusi, serikali ya Syria imekataa kutoa fursa kwa Umoja wa mataifa kuingia Mashariki mwa Aleppo na Mashariki mwa Ghouta karibu na mji wa Damascus, huo uamuzi ni lazima ubadilishwe ameongeza..