Skip to main content

Wakaguzi, wahasibu wanawezesha ukwepaji kodi duniani- Mtaalamu

Wakaguzi, wahasibu wanawezesha ukwepaji kodi duniani- Mtaalamu

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kodi, Alfred de Zayas amesema kiwango cha ukwepaji kodi duniani ni cha kutisha.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa, de Zayas amesema kitendo hicho cha ukwepaji kodi kinagharimu serikali kote ulimwenguni karibu dola Trilioni Tatu kila mwaka licha ya kwamba serikali zinategemea kodi ili kuendeleza uchumi na kutoa huduma za kijamii.

(Sauti ya de Zayas)

“Tatizo ni kwamba tuna mfumo wa ukwepaji kodi ambapo wakaguzi, kampuni za uhasibu, wanasheria, wabunge wote wako kwenye mchezo huu na wote wanapata pesa,. Ni jambo la kustaajabisha kwamba kampuni nne kubwa za uhasibu wako kwenye mchezo huu na ndio zinazotunga kanuni.”

Ili kudhibiti ukwepaji huo wa kodi ambao unaweza kukwamisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na hata mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, de Zayas anataka Umoja wa Mataifa uanzishe mamlaka ya kimataifa ya kodi ili kuepusha ukwepaji kodi na rushwa akisema..

(Sauti ya de Zayas)

“Umoja wa Mataifa ndio chombo pekee cha kimataifa kinachoweza kubeba jukumu hili, lakini kile kinachokosekana ni utashi wa kisiasa.”