Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

António Guterres ni nani?

António Guterres ni nani?

Wengi wanajiuliza António Guterres aliyepitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwania kuwa Katibu Mkuu wa Tisa wa chombo hicho ni nani? Guterres ni raia wa Ureno ambaye mwaka 2005 alichaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Kamishna Mkuu wa shirika la umoja huo la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Jukumu lake hilo la ukamishna lilikamilika mwaka 2015 ambapo kabla ya kujiunga na Umoja wa Mataifa alihudumu katika serikali ya Ureno kwa zaidi ya miaka 20 akishikilia nyadhifa mbali mbali ikiwemo Uwaziri Mkuu kati ya mwaka 1995 hadi 2002.

Guterres ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 67, aliasisi baraza la wakimbizi la Ureno mwaka 1991 na kwa muda alishikilia urais wa Baraza la Umoja wa Ulaya mwaka 2000.

image
Antonio Guterres akiwa na Katibu Mkuu Ban Ki-moon wakikutana na waomba hifadhi.(Picha:UM/NICA)
Akiwa Kamishna Mkuu wa UNHCR alisimamia mchakato mkubwa wa marekebisho ya kimuundo ikiwemo kujenga uwezo wa shirika hilo kushughulikia majanga makubwa ya wakimbizi kuwahi kushuhudiwa baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Alisafiri kona mbali mbali za dunia kuzungumza na wakimbizi na kushuhudia madhila wanayoyapata.

Mathalani alifika huko Molivos, Ugiriki, ambako alikutana na wakimbizi wanaosaka hifadhi barani Ulaya ambapo baada ya kuzungumza nao alisema..

“Iwapo mwenendo utasalia huu wa shaghalabaghala kama ilivyo hivi sasa, itakuwa vigumu sana kuepusha majanga wakati wa msimu wa baridi kali. Tunafahamu jinsi ya kuweka mazingira murua kwenye majira ya baridi ndani ya hema, ndani ya kambi na hata kwenye kituo cha mapokezi. Lakini ni vigumu kutoa huduma hiyo kwwa umati wa watu unaohama kutoka nchi moja kwenda nyingine wakati wa baridi kali, theluji na vimbunga.”

Miongoni mwa ahadi alizotoa wakati wa mchakato wa kusaka Ukatibu Mkuu ni pamoja na kuimairisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Afrika ambapo alisema..

(Sauti ya Guterres)

“Kwangu mimi, ushirikiano na Muungano wa Afrika bila shaka ni lazima. Na unapaswa kuwa katika misingi ya uwazi na kuaminiana.”

Aliangazia pia suala la mikutano inayofanyika ndani ya Umoja wa Mataifa akisema..

(Sauti ya Guterres)

“Hebu tuwe wazi. Tuna mikutano mingi, watu wengi wakijadili masuala mengi lakini matokeo kidogo. Na naamini tunahitaji kuondokana na mfumo huu na kuwa na mfumo unaoleta matokeo.”

image
Antonio Guterres akiwa na Koffi Annan.( Picha:UM/NICA)