Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na nchi za Afrika wakubaliana hatima ya wakimbizi wa Rwanda,

UNHCR na nchi za Afrika wakubaliana hatima ya wakimbizi wa Rwanda,

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na ujumbe kutoka nchi za Afrika , pamoja na Muungano wa Afrika ijumaa wameafikiana hatua za mwisho za kumaliza suala lamuda mrefu la wakimbizi wa Rwanda baada ya miaka saba ya majadiliano.

Mkutano wa mawaziri ulioandaliwa na UNHCR mjini Geneva , umekamilisha hatua ya mwisho ya mchakato wa kina wa mikakati ya suluhu kwa ajili ya wakimbizi wa Rwanda ambao walifungasha virago kati yam waka 1959 na 1998, kukimbia machafuko ya kikabila na vita.

Akizungumzia hatua hiyo mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema katika dunia ambayo ina zaidi ya wakimbizi milioni 21, mtazamo usiwe tuu kuwapa ulinzi na msaada wa kibinadamu, lakini katika kusaka suluhu.

Ameongeza kuwa mkutano huo umefikia hatua kubwa ya kutoa suluhu kwa maelfu ya Wanyarwanda walioomba hifadhi ya ukimbizi 1959 na 1998 na hivyo kulifikisha ukiongi moja la tatizo la muda mrefu la wakimbizi Afrika.

Washiriki wa mkutano huo ambao wametoka Rwanda na nchi zinazohifadhi wakimbizi hao za Angola, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Kenya, Malawi, Jamhuri ya Congo, Afrika Kusini, Uganda, Zambia na Zimbabwe wamesisitiza nia yao ya kuhakikisha wanakamilisha mchakato huo ulioanza Oktoba mwaka 2009 , ifikapo mwisho wa mwaka ujao.