Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utoaji mimba usio salama bado unakatili maisha ya maelfu ya vigori duniani:UM

Utoaji mimba usio salama bado unakatili maisha ya maelfu ya vigori duniani:UM

Wakizungumza kabla ya siku ya kimataifa ya hatua za kuhakikisha fursa ya utoaji mimba salama na uliohalalishwa kisheria, kundi la wataalamu wa haki za binadamu, wametoa wito kwa nchi duniani kufuta sera na sheria zinazopinga utoaji mimba, adahabu zozote na vikwazo ambavyo vitawanyima fursa ya huduma ya afya ya uzazi.

Wataalamu hao pia wamesema wanaunga mkono wito wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali wa kuifanya tarehe 28 Septemba kuwa siku rasmi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya utoaji mimba salama duniani, na kuzitaka nchi kutoharamisha utoaji mimba na kutoa huduma za afya ya uzazi katika njia halali, salama na ya gharama nafuu.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO takribani visa milioni 22 vya utoaji mimba usio salama hufanyika kila mwaka duniani kote na inakadiriwa kwamba wanawake 47,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na athari za utoaji mimba usio salama.