Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo wa Syria waanika udhaifu wa Baraza la Usalama la UM-Zuma

Mzozo wa Syria waanika udhaifu wa Baraza la Usalama la UM-Zuma

Mkwamo ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kusaka suluhu ya mzozo wa Syria unatoa fursa ya kuhoji iwapo baraza hilo lina uwezo wa kushughulikia changamoto za usalama za karne ya sasa.

Ni kauli ya Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini katika hotuba yake kwenye mjadala wa wazi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo.

Amesema miaka mitano sasa hakuna nuru ya kumalizika kwa mzozo huo ambao unaendelea kuathiri ukanda husika.

(Sauti ya Zuma)

“Mkwamo ndani ya Baraza la Usalama kuhusu suala la Syria, unaanika muundo usiofanya kazi wa chombo hicho uliopitishwa mwaka 1945 baada ya makubaliano kufuatia kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia."

Hivyo akahoji..

(Sauti ya Zuma)

“Tunapaswa kujiuliza iwapo Umoja wa Mataifa na hususan Baraza la Usalama na muundo wake wa sasa linaweza kukidhi majukumu yake katika kushughulikia changamoto za karne ya 21. Baraza la Usalama linapaswa kuchukua hatua za pamoja badala ya kuyumbishwa na maslahi ya kitaifa ya nchi chache.”

Na katika kuhakikisha bara la Afrika linafanikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, Rais Zuma amepazia sauti utoroshaji haramu wa fedha kutoka Afrika ambao kwa mwaka hukaribia dola Trilioni 50.

(Sauti ya Zuma)

“Tunasihi jamii ya kimataifa ishughulikie suala hili kwa udharura wake unaostahili.”