Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msafara wa misaada washambuliwa huko Aleppo

Msafara wa misaada washambuliwa huko Aleppo

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura amethibitisha kutokea kwa shambulio dhidi ya magari 18 kati ya 31 yaliyokuwa kwenye msafara wa kupeleka misaada ya kibinamu huko Aleppo, Syria.

Taarifa kutoka ofisi yake imeeleza kuwa hadi sasa wanatathmini iwapo shambulio hilo kwenye eneo la Big Orem magharibi mwa Aleppo, lililikuwa ni la kutoka angani au la kombora.

Inaelezwa kuwa msafara huo wa  wadau wa Umoja wa Mataifa na shirika la msalaba mwekundu la Syria, SARC ulishambuliwa Jumatatu jioni.

Bwana Staffan amechukizwa na shambulio hilo akisema msafara huo uliwezekana kufanyika baada ya majadiliano ya muda mrefu ya kusaka vibali ili kuweza kufikia raia walio pembezoni.

Naye Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya dharura, OCHA, Stephen O’Brien amesema tukio hilo limemsikitisha na ametaka pande zote kwenye mzozo kuchukua hatua zote kulinda watoa misaada ya kibinadamu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.