Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na #GMG wapigia chepuo azimio la New York

UNICEF na #GMG wapigia chepuo azimio la New York

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema kupitishwa kwa azimio la New York, kuhusu wakimbizi na wahamiaji ni hatua ya kwanza ya kushughulikia wimbi kubwa la hamahama ya watu ambayo dunia haijawahi kushuhudia.

Taarifa ya UNICEF imesema azimio hilo ambalo linaweka hatua za kimsingi za kuchukuliwa kulinda makundi hayo, litaokoa mamilioni ya watu wakiwemo watoto ambao wakati huu ni nusu ya wakimbizi duniani.

Kwa mantiki hiyo UNICEF imesema katika miaka miwili ijayo itashirikiana na nchi wanachama, wadau wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na watoto kutangaza hatua dhahiri za kulinda watoto wanaong’oka makwao kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo mizozo.

Naye Phumzile Mlambo-Ngucka, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN-Women akizungumza kwa wadhifa wa uenyekiti wa kundi la kusaka suluhu la wahamiaji, Global Migration Group, #GMG baada ya kupitishwa azimio la New York, amesema..

(Sauti ya Phumzile)

"Kundi hili linasimama pamoja na kusaidia wale wanaoteseka na kudhalilishwa, kundi hili la uhamiaji duniani linasimama pamoja na nchi wanachama, mashirika ya kiraia na wadau chini ya ajenda ya maendelee endelevu kwa ajili ya maendeleo endelevu."