Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFRC yapeleka wasaidizi Bukoba, UNISDR yasema ni vigumu kubashiri tetemeko

IFRC yapeleka wasaidizi Bukoba, UNISDR yasema ni vigumu kubashiri tetemeko

Kufuatia tetemeko la ardhi mkoani Kagera nchini Tanzania, shirikisho la msalaba mwekundu na hilal nyekundu, IFRC, limepeleka zaidi ya wafanyakazi 50 wa kujitolea na watendaji wake ili kufanikisha usaidizi kwa wahanga wa tukio hilo.

Mkurugenzi wa IFRC kanda ya Afrika Fatoumata Nafo-Traore amesema wamechukua hatua hiyo kwa kuwa hospitali zimezidiwa uwezo na watu wanahitaji msaada ikiwemo chakula.

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya upunguzaji wa hatari ya majanga UNISDR imesema kwa kuwa ni vigumu kubashiri kutokea kwa tetemeko la ardhi, lakini linaloweza kufanyika..

(Sauti ya Amjad)

“Kuhakikisha tunaandaa na kusimamia kanuni sahihi za majengo ambayo yanaweza kustahimili aina ya tetemeko linaloweza kutokea.”

Amepongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC kwa kuandaa sheria ya kupunguza athari za majanga ikiwemo matetemeko ya ardhi akisema..

(Sauti ya Amjad)

“Hatua inayofuatia ni kwa waamuzi katika ngazi ya taifa kutafsiri muswada huo uwe mkakati wa kitaifa wa kudhibiti majanga.”

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa tetemeko la ardhi kwenye ukanda huo wa bonde la ufa hutokea kila baada ya miaka 10 lakini la sasa limesababisha vifo vingi na madhara zaidi kuliko idadi ya matetemeko yaliyotokewa miaka 100 iliyopita.