Mwendazake Margaret Anstee kuzikwa kesho, Ban atuma rambirambi
Nimesikitishwa sana na kifo cha Margaret Anstee, mwanamke wa kwanza kuteuliwa kwenye safu za juu katika Umoja wa Mataifa.
Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika salamu za rambirambi kufuatia taarifa za kifo cha Dame Anstee ambaye alihudumu kwenye umoja huo kwa miongo minne na kushika nyadhifa kadhaa ikiwemo msaidizi wa Katibu Mkuu, akiwa mwanamke wa kwanza. Anstee alikuwa pia mwanamke wa kwanza kuongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Angola, UNAVEM II mwaka 1992.

Mathalani alijitolea kwa miaka mingi kufanya kazi katika mazingira magumu katika maeneo mbali mbali ikiwemo kusambaza misaada kwenye maeneo ya majanga kama vile Bangladesh na Mexico, na kusaidia watoto wa Chernobyl baada ya ajali ya nyuklia.
Katibu Mkuu amesema Bi. Anstee alijitambua nafasi yake na hivyo kamwe hakuchelea kujiweka hatarini katika kufanikisha jambo na alisihi wanawake wenzake kujaribu fursa na kusaidiana.

Bi. Anstee ambaye alifariki dunia tarehe 25 mwezi uliopita, atazikwa kesho Ijumaa. Alizaliwa mwaka 1926 huko Uingereza na alijiunga na Umoja wa Mataifa mwaka 1952 hadi 1993..