UNMISS yahofia kunyanyaswa kwa NGOs Sudan Kusini
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS una wasiwasi kufuatia ripoti za kuwepo kwa vitisho na unyanyasaji dhidi ya baadhi ya wanachama wa mashirika ya kiraia waliokutana na ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yao ya hivi karibuni mjini Juba.
Taarifa ya UNMISS imesema vitendo hivyo ukiukwaji wa haki za uhuru wa kujieleza, harakati na ushiriki wa kiraia na kisiasa, ambazo ni nguzo ya msingi ya jamii ya kidemokrasia.
UNMISS imelaani jaribio lolote la kukandamiza haki hizo kwa njia ya vitisho na unyanyasaji.
Ikaongezea kwa kusema kuwa kukutana na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ilikuwa fursa kwa mjadala wa wazi kwa lengo la kupata kuelewa baadhi ya masuala na hoja zinazowakabili wananchi wa Sudan Kusini hadi ngazi za chini.
Kwa mantiki hiyo UNMISS imesema itawasilisha hofu yake kwa mamlaka zote husika.