Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zerrougui ataka hatua madhubuti kuwalinda watoto walioathiriwa na mzozo Somalia

Zerrougui ataka hatua madhubuti kuwalinda watoto walioathiriwa na mzozo Somalia

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto na mizozo ya silaha, Leila Zerrougui, ametoa wito hatua madhubuti zichukuliwe ili kuwalinda watoto dhidi ya kusajiliwa na kutumikishwa na vikosi au vikundi vyenye silaha nchini Somalia.

Bi Zerrougui ameutoa wito huo mwishoni mwa ziara yake ya pili nchini Somalia, ambako ametoa wito kwa mamlaka za nchi hiyo kuwachukulia watoto wanaoshukiwa kuhusiana na Al-Shabaab kama waathiriwa, na kuzingatia maslahi ya watoto chini ya viwango na kanuni za kimataia kuhusu ulinzi wa watoto.

Amesema watoto nchini Somalia wanakabiliwa na hali ngumu, hususan kusajiliwa na kutumikishwa vitani, pamoja na kutekwa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Ameongeza kuwa licha ya mazingira magumu, serikali ya Somalia imechukua hatua muhimu katika miaka ya hivi karibuni kuwalinda watoto, kwa kuridhia mkataba kuhusu haki ya mtoto, na kutia saini mipango tekelezi miwili ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia usajili na utumikishaji wa watoto, kuwaua na kuwalemaza.