Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

“Kutoka uamuzi hadi utekelezaji”; UNCTAD 14 yaoana vyema na SDGs- Ban

“Kutoka uamuzi hadi utekelezaji”; UNCTAD 14 yaoana vyema na SDGs- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema ingawa kumekuwa na mabadiliko mengi duniani tangu mkutano wa nne wa Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) uliofanyika jijini Nairobi miongo minne iliyopita, changamoto zilizotajwa katika mkutano huo bado zipo kwenye ajenda ya kimataifa.

Ban amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 14 wa UNCTAD, ambao unafanyika Nairobi, Kenya kuanzia leo Julai 17 hadi Julai 22.

Katibu Mkuu amesema udhoofu wa nchi zenye maendeleo duni katika masoko ya bidhaa ulimulikwa katika UNCTAD IV, na bado ni suala linaloendelea kuwepo hata sasa, ikiwa kasi ya biashara duniani imefifia, huku bei za bidhaa zikiwa zimeshuka.

“Unyonge wa masoko ya kimataifa unatokana, siyo tu na masoko yasiyotabirika na misukosuko ya kijamii, bali unatokana pia na mazingira hafifu ya kimataifa yaliyodhoofishwa hata zaidi na mabadiliko ya tabianchi.”

Katibu Mkuu amesema kauli mbiu ya UNCTAD 14, ya “kutoka uamuzi hadi kuchukua hatua”, inafaa, kwani UNCTAD 14 ndio mkutano wa kwanza mkubwa wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo, tangu kupitishwa kwa Ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) na Ajenda ya Addis Ababa ya kuchukua hatua kuhusu ufadhili kwa ajili ya maendeleo, na kwamba mwaka huu, nchi zimeanza jukumu la utekelezaji.

“Lakini hatua fanisi tutakazohitaji katika miaka 15 ijayo – hususan katika Nyanja za biashara, uwekezaji, teknolojia na ufadhili – zinahitaji tutumie uwezo wa wadau wote, tuendeleze uvumbuzi, na kurekebisha mienendo isiyo endelevu. Ujumbe wangu kwenu leo ni kwamba SDGs zinawakilisha mabadiliko tunayohitaji ili kurejesha imani ya watu katika uchumi wa kimataifa”

Ban amesema SDGs zinatoa fursa kubwa ya kuufanya uchumi uwe wenye hadhi kwa wote, utajiri kwa wote, na sayari bora kwa wote