Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Sudan Kusini mnakatisha tamaa jamii inayowasaidia- Ban

Viongozi wa Sudan Kusini mnakatisha tamaa jamii inayowasaidia- Ban

Akiwa nchini Kenya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, wamezungumza na waandishi habari ambapo wamegusia masuala kadhaa ikiwemo amani na usalama Burundi halikadhalika nchini Sudan Kusini.

Mkutano huo umefanyika Ikulu ya Nairobi, ambapo Ban ameshukuru uongozi wa Rais Kenyattta katika kusaka suluhu la mzozo huo wa Sudan Kusini uliosababisha watu kukimbilia nchi jirani ikiwemo Kenya, huku akisema..

(Sauti ya Ban-1)

"Nimekuwa nawasihi viongozi wa Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani ina miaka mitano tu, wanapaswa kuchukua hatua zaidi kwa taifa lao. Viongozi wa nchi hii wanakatisha tamaa jamii ya kimataifa ambayo imekuwa ikiwasaidia. Nimewasihi na naendelea kuwasihi wasikilize sauti ya dunia."

image
Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon akizungumza Ikulu ya Nairobi. (Picha:Newton Kanhema/UNIC Nairobi)
Ban akaelekeza hotuba yak ekwa viongozi wa Sudan Kusini.

(Sauti ya Ban-2)

"Raia wanavyoendelea kukimbia mapigano Sudan Kusini na maeneo ya jirani ikiwemo kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya, napongeza Kenya kwa ukarimu wake na wananchi wake."

Rais Kenyatta naye pamoja na mambo mengine akazungumzia kinachoendelea Sudan Kusini

(Sauti- Uhuru-1)

"Hakika ndugu yetu mwenye umri mdogo zaidi katika ukanda wetu na duniani, ametumbukia tena kwenye mgawanyiko na ghasia, na ni wajibu wetu, sisi sote, lakini hususan kwenye ukanda huu kurejesha amani na hakika iwe ya kudumu."

image
Wana habari wakinasa picha na ripoti kwenye mkutano huo. (Picha:Newton Kanhema/UNIC Nairobi)
Halikadhalika wajibu kwa jamii ya kimataifa akielekeza zaidi kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Uhuru-2)

"Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mushauri kwa ufasaha zaidi mamlaka ya UMISS, ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini ili uweze kutenganisha wale waliojitumbukiza kwenye ghasia, ili uweze kulinda miundombinu ya Sudan Kusini, na muhimu zaidi uweze kulinda wananchi wa Sudan Kusini ili wajenge amani na kuilinda, na hiyo ndiyo maana ya kuwajibika kwa pamoja."