Akiwa Rwanda Ban akutana na Kagame; wajadili Sudan Kusini, Burundi na tabianchi

Akiwa Rwanda Ban akutana na Kagame; wajadili Sudan Kusini, Burundi na tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ambaye yuko ziarani nchini Rwanda kuhudhuria kikao cha Muungano wa Afrika (AU), amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambapo Ban amempa heko Rais huyo kwa uongozi wake na kwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa AU.

Ban ametoa shukrani zake kwa mchango wa Rwanda katika masuala ya ulinzi wa amani, hususan katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Darfur Sudan, na Sudani Kusini.

Katibu Mkuu na Rais Kagame wameelezea masikitiko yao kuhusu kuibuka na kuongezeka machafuko Sudan Kusini, athari zake kwa raia, na kwa mchakato wa amani.

Wametoa wito kwa viongozi wa Sudan Kusini waonyeshe dhamira inayohitajika ili kukomesha janga linaloibuka nchini mwao, na kutimiza matamanio ya watu wa Sudan Kusini kuhusu amani na maridshiano.

Aidha, viongozi hao wamebadilishana mawazo kuhusu masuala mengine, ikiwemo hali nchini Burundi, huku Ban akitoa shukrani zake kwa Rwanda kwa kuwapa hifadhi maelfu ya wakimbizi wa Burundi.

Hatimaye, Ban ameelezea matarajio yake kuwa Rwanda itaridhia Mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi kabla ya mwisho wa mwaka huu.