Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto bado ni kubwa Chad, msaada wahitajika:OCHA

Changamoto bado ni kubwa Chad, msaada wahitajika:OCHA

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini  Chad Stephen Tull, akiwa na mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA Florent Méhaule, wamezuru Abeche,jimbo la Ouaddai wiki iliyopita.

Wakiwa jimboni humo wameshuhudia hali halisi ya mahitaji ya kibinadamu na maendeleo hasa Mashariki mwa Chad. Wamesema watu chini ya asilimia 30 ndio wanaoweza kupata maji safi ya kunywa, karibu robo ya watu wote hawana uhakika wa chakula na kiwango cha utapiamlo kimepindukia hali ya tahadhari.

Wamesema matatizo mengine yanayowakabili watu wa eneo hilo ni huduma za msingi kama elimu na afya. Ujumbe huo umeongeza kuwa ni muhimu kuwekeza katika msaada wa kibinadamu na maendeleo kunusuru watu hawa.