Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa, UNICEF walaani mashambulio Baghdad

Umoja wa Mataifa, UNICEF walaani mashambulio Baghdad

Huko Baghdad, nchini Iraq mashambulio ya kigaidi yamesababisha vifo vya watu 125 na majeruhi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amelaani mashambulio hayo ya leo.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Ban akieleza kuchukizwa na kitendo cha ukosefu wa ubinadamu uliodhihirishwa na watekelezaji wa mashambulio hayo wakati watu walipokuwa wakijiandaa na shamrashamra za Eid al-Fitr.

Ametuma rambirambi kwa wafiwa na serikali ya Iraq huku akiwatakia ahueni ya mapema majeruhi.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa wananchi wa Iraq kukataa majaribio yoyote ya kueneza hofu sanjari na mipango yoyote ya kudumaza umoja wa nchi hiyo.

Wakati huo huo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft naye amelaani mashambulio hayo ya kigaidia akisema ghasia za kutisha dhidi ya watu wakiwemo watoto wakati huu wa mfungo wa Ramadhani zinapaswa kulaani kwa njia zote.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa taarifa kufuatia shambulio hilo likisema miongo minne ya mzozo Iraq umesababisha nchi hiyo kuwa eneo hatari zaidi duniani kwa watoto.

UNICEF imesema kadri ghasia zinavyoshika kasi Iraq, watoto wanaendelea kubeba mzigo wa madhara na kwamba kuua au kusababisha ulemavu kwa watoto ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kibinadamu za kimataifa.