Kuna haja ya kuimarisha mifumo ya afya kukabiliana na dharura za kiafya- Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema ripoti zilizochapishwa na jopo la ngazi ya juu kuhusu jitihada za kimataifa wakati wa mizozo ya kiafya, zinabainisha moja ya changamoto za dharura na za muda mrefu zaidi katika nyakati za sasa.
Ban amesema, mnamo mwezi Februari mwaka huu, jopo hilo lilichapisha ripoti iliyotoa mapendekezo 27 ya hatua za kuchukua kwenye ngazi za kitaifa, kikanda, na kimataifa.
Jopo hilo lilisisitiza kuwa kuifanya mifumo ya afya iwe imara zaidi na tayari kwa dharura kunahitaji utafiti na maendeleo vumbuzi, ufadhili tosha, na uungwaji mkono kupitia mipango ya maendeleo.

Akizungumza kwa njia ya video kutoka jijini Dakar, Senegal, mwenyekiti wa jopo hilo ambaye ni Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amesema jopo hilo lilibaini kuwa mlipuko wa Ebola uliweka dhahiri udhaifu mkubwa katika mfumo wa kimataifa wa afya.

Aidha amesema jopo hilo lilibaini kuwa mifumo ya afya katika nchi zenye maendeleo duni ni dhaifu.
“Kwa hiyo nchi hizo zinakabiliwa na hatari iwapo kutakuwa na milipuko ya magonjwa, kwa sababu zina uwezo mdogo wa kuizuia au kuishughulikia. Hili lilidhihirishwa Liberia, Guinea na Sierra Leone.”