Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO inasema ni salama kusafiri licha ya kusambaa kwa homa ya H1N1 duniani

WHO inasema ni salama kusafiri licha ya kusambaa kwa homa ya H1N1 duniani

Msemaji wa WHO, Fadela Chaib alinakiliwa pia kuonya kwenye taarifa yake mbele ya waandishi habari wa kimataifa Geneva, kwamba ijapokuwa ilani ya tahadhari juu ya maambukizo ya homa ya mafua ya H1N1 ipo kwenye kiwango cha 5 kwa sasa, uamuzi huu wa WHO haumaanishi katu watu wanaotaka kusafiri, nje ya maeneo yao, wanyimwe haki ya kusafiri.

 Alikumbusha, UM hutoa ilani za tahadhari aina kwa aina, baada ya kufanyika uchunguzi wa kisayansi. Matokeo ya fafanuzi za karibuni yameshatathminia kihakika kama janga la maradhi ya homa limepevuka kimataifa na yamethibitisha hakuna hatari kwa umma kusafiri nje ya maeno yao. Alisema kwa sasa virusi vya homa ya H1N1 vimeshasambaa katika nchi mbalimbali za dunia, na kwa hivyo WHO haioni kuna hoja ya maana yoyote ya kuwahamasisha wenye madaraka kupiga marufuku watu kusafiri nje ya maeneo yao au kwa mataifa kufunga mipaka. Alihadharisha pindi hatua hizi zitachukuliwa, hazitosaidia kamwe kwenye zile juhudi za kudhibiti virusi kutoenea kimataifa, hali ambayo natija yake itakuwa ni kuzusha mtafaruku tu, utakaosambaratisha pakubwa maisha ya kawaida ya jamii ya kimataifa.