Skip to main content

Kubinya baadhi ya sekta ni kikwazo kwa maendeleo- Ban

Kubinya baadhi ya sekta ni kikwazo kwa maendeleo- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ushirikiano baina ya serikali na taasisi nyingine ikiwemo zile za kiraia ni muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu.

Ban amesema hayo akizungumza kwenye mkutano wa kimataia wa uchumi huko St. Petersburg nchini Urusi, huku hata hivyo akieleza masikitiko yake juu ya madhila wanayokumbana nayo taasisi za kiraia na vyombo vya habari.

Mathalani ametaja sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari halikadhalika uhuru wa watetezi wa haki za binadamu na na upatiaji fedha mashirika ya kiraia.

“Kuna kubinywa kwa fursa ya kidemokrasia kwa mashirika ya kiraia na hii inakwamisha kwa kweli maendeleo endelevu ya jamii zetu.Kubana vyombo vya habari kunanyamazisha tu sauti ambazo tunahitaji ili kuwajibisha viongozi na ndipo mashirika ya kiraia nayo yaweze kutekeleza majukumu yao vyema kwa manufaa ya jamii nzima..”

Katibu Mkuu amesema zama za sasa ni za mizozo lakini bado ni zama za fursa na kwamba Umoja wa Mataifa unatarajia kushirikiana na sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wadau wote ili kukabili changamoto za sasa na kusongesha mbele ajenda za mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ili kuwa na mustakhbali wenye utu kwa wote.