Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni mpya ya UNHCR yataka ulimwengu ushikamane na wakimbizi

Kampeni mpya ya UNHCR yataka ulimwengu ushikamane na wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR), limezindua leo kampeni inayoutaka ulimwengu uonyeshe mshikamano na wakimbizi.

Kampeni hiyo ni kupitia ujumbe wa video, ambapo zaidi ya watu 60 maarufu kutoka kote duniani wanaungana na wakimbizi na wahudumu wa kibinadamu, wakitoa wito kwa serikali zichukue hatua kwa ajili ya wakimbizi, kwa kupaza ujumbe, “tunashikamana na wakimbizi, tafadhali shikamana nasi”

Miongoni mwa nyota waliomo kwenye video hiyo ni mwanamitindo Alek Wek, ambaye zamani alikuwa mkimbizi, waigizaji filamu Cate Blanchett, ambaye ni Balozi mwema wa UNHCR, Benedict Cumberbatch, Chiwetel Ejiofor, Margot Robbie, Ben Stiller, Dame Helen Mirren na waimbaji Juanes, Mika, Maher Zain and Babaa Maal.

(Sauti zao)

Hapa wanasema katika lugha mbalimbali, “Tunashikamana na wakimbizi”

Kampeni hiyo inayomjumuisha Katibu Mkuu Ban Ki-moon na Askofu Desmond Tutu, inalenga kuonyesha uungaji mkono kwa familia zilizolazimika kuhama makwao, katika muktadha wa kuongezeka kwa wakimbizi kutokana na mizozo na ukatili, huku kukiwa na kauli zinazochochea chuki dhidi ya wakimbizi na wahamiaji.