Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu ulemavu wa ngozi kuadhimishwa-UNESCO

Siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu ulemavu wa ngozi kuadhimishwa-UNESCO

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu ulemavu wa ngozi hapo Juni 13, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, linaandaa tukio maalumu liitwalo “kuishi na ulemavu wa ngozi” kwa lengo la kuelimisha kuhusu hali hiyo ya kuzaliwa nayo ambayo mara nyingi hukabiliwa na ubaguzi.

Tukio hilo linaambatana na mkutano unaojikita katika mtazamo wa dawa katika ulemavu wa ngozi utakaowaleta pamoja wataalamu wa afya, wataalamu wa ngozi na masuala ya kijenetiki, na watajadili na kuorodhesha yapi yanayofahamika hadi sasa kuhusu ulemavu wa ngozi ugonjwa unaosababishwa na upungufu wa madini yanayoleta rangi ya ngozi yaani melanin.

Wengine watakaojumuishwa kwenye mjadala ni wawakilishi wa asasi za kiraia za watu wenye ulemavu wa ngozi. Pia kutaonyeshwa filamu fupi iitwayo “Mtu mweusi , ngozi nyeupe” ( Black man, white skin) iliyoandaliwa na José Manuel Colón, pia maonyesho ya picha zilizoandaliwa na Patricia Willocq .