Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu wa kingono vitani wahitaji hatua zaidi: Bangura

Uhalifu wa kingono vitani wahitaji hatua zaidi: Bangura

Leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili ukatili wa kingono vitani, Katibu Mkuu akisema kwamba janga hilo ambalo linatumiwa kama silaha ya vita hivi limeenea duniani kote. Taarifa zaidi na Grace Kaneyia.

(Taarifa ya Grace)

Akihutubia mkutano huo, Bwana Ban amemulika mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na ukatili wa kingono vitani, ikiwemo kupitia washauri maalum wa kike wanaosambazwa kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa ili kufuatilia visa hivyo .

Hata hivyo amesema changamoto ni nyingi, akitaja vikundi vya kigaidi vya Daesh au Boko Haram ambao wanatumia ukatili wa kingono kuvutia wapiganaji na kuzalisha kipato pia.

Kwa upande wake Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu kuhusu ukatili wa kingono vitani Zainab Hawa Bangura ameeleza jinsi ukatili huo umebadilika hadi kuwa sasa biashara ya utumwa, nyenzo ya utawala, tishio kwa raia na shinikizo la kisiasa.

Akisihi Baraza la Usalama kuchukua hatua thabiti ili kupambana na janga hilo akasema

(Sauti ya Bangura)

"Manusura wakisema miili yetu ina thamani ndogo kuliko panya aliyekufa, inapunguza ubinadamu wetu wa pamoja. Hatimaye, maneno yetu yote, sheria, na maazimio, hayatakuwa na maana iwapo uhalifu hauadhibiwi na iwapo hatutaweza kuongeza gharama na madhara ya kutenda uhalifu huo.”