Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa wakuu wa polisi duniani waanza leo New York

Mkutano wa wakuu wa polisi duniani waanza leo New York

Mkutano wa aina yake wa wakuu wa polisi kutoka nchi 109 wanachama wa Umoja wa Mataifa unaanza leo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani.

Miongoni mwa malengo ya mkutano huo ni kutoa fursa kwa wakuu wa majeshi ya polisi kujadili jinsi ya kuimarisha vikosi vya polisi vya Umoja wa Mataifa vinavyoshiriki katika operesheni za ulinzi wa amani ili viweze kukabiliana na changamoto za karne ya sasa.

Mkutano huo unafanyika huku kukiwa kumetolewa ripoti ya tathmini iliyofanywa miezi sita na jopo la nje kuhusu kitengo cha polisi cha Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine inameangalia changamoto za operesheni za ulinzi wa amani zinazotekelezwa na polisi ambapo Hilde Johnson ambaye ni mwenyekiti mwenza wa jopo hilo anaelezea baadhi ya mambo waliyobaini..

(Sauti ya Hilde)

 “Dhima kuu na majukumu ya Polisi haitambuliwi katika mfumo wa Umoja wa Mataifa. Mara nyingi majukumu ya kijeshi yanapatiwa kipaumbele, na hili kwenye jopo la tathmini limeonekana ni jambo la kusikitisha.”

Hivyo akataja miongoni mwa mapendekezo.

(Sauti Hilde-2)

“Kuna umuhimu wa kuwepo kwa usawa kati ya polisi na jeshi  katika operesheni za ulinzi wa amani, kwenye makao makuu na pia mashinani. Na tunapendekeza nafasi ya mshauri wa polisi ipandishwe cheo iwe msaidizi wa katibu Mkuu, ASG.”

Ripoti pia imependekeza mipango ya ulinzi wa amani na mamlaka za polisi izingatie tathmini ya kina ya hali ya kisiasa na mahitaji ya kiufundi ya eneo husika.

Miongoni mwa nchi zitakazoshiriki mkutano huo wa wakuu wa polisi ni Rwanda, Uganda na Tanzania.