Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wataka watoto waliotekwa Gambella, Ethiopia waachiwe huru

Wataalam wa UM wataka watoto waliotekwa Gambella, Ethiopia waachiwe huru

Wataalam wawili wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, wametoa wito kwa mamlaka za Ethiopia na Sudan Kusini ziongeze juhudi za kuachiwa huru watoto wote waliotekwa kutoka jimbo la Gambella, magharibi mwa Ethiopia, lilipovamiwa na watu wenye silaha kutoka Sudan Kusini.

Mnamo Aprili 15, 2016, watu 208 waliripotiwa kuuawa, huku wasichana na wavulana 146 wakitekwa na wanaume wenye silaha kutoka kabila la Murle, walipovuka mpaka kutoka Sudan Kusini na kuvamia vijiji 13 vya kabila la Nuer katika wilaya za Jiksaw na Lare, jimbo la Gambella, nchini Ethiopia.

Watu 80 waliripotiwa kujeruhiwa wakati wa uvamizi huo, na ng’ombe zaidi ya 2,000 kuibwa.

Wito wa wataalam hao wa Umoja wa Mataifa, ambao ni Maud de Boer-Buquicchio, anayehusika na uuzaji wa watoto, na Christof Heynz, anayehusika na mauaji holela, unakuja baada ya ripoti za watoto 59 waliotekwa kukombolewa na kurejeshwa Ethiopia wiki iliyopita.

Wengi wa watoto waliokombolewa ni chini ya umri wa miaka 13.