Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za Tanzania kwenye uchumi zinazaa matunda- Benki ya Dunia

Hatua za Tanzania kwenye uchumi zinazaa matunda- Benki ya Dunia

Hatua za kukwamua uchumi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya Tano nchini Tanzania zimeanza kuzaa matunda ikiwemo ongezeko la makusanyo ya mapato ya kila mwezi. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Benki ya Dunia katika ripoti yake ya nane iliyotolewa leo kuhusu uchumi wa Tanzania imetaja hatua hizo kuwa ni pamoja na udhibiti wa matumizi ya fedha na rushwa.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkazi wa benki hiyo nchini Tanzania Bella Bird amesema mafanikio hayo yatakuwa endelevu iwapo serikali itawekeza zaidi kwenye miundombinu na rasilimali watu kama njia ya kuweka mazingira bora ili sekta binafsi ichanue zaidi na kufungua ajira.

Amesema hatua hiyo siyo tu itapunguza umaskini kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu, bali pia itaendana na vipaumbele vya serikali ya sasa na azma yake ya kufanikisha dira ya 2025.

Ripoti inagusia pia ubia kati ya serikali na sekta binafsi, PPP ikisema ni hatua njema lakini mipango madhubuti inatakiwa ili kuondokana na tabia ya utendaji kazi kwa mazoea katika ubunifu na utekelezaji wa PPP.