Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gordon Brown kuzindua mfuko bunifu wa ufadhili kwa elimu ya watoto wakimbizi

Gordon Brown kuzindua mfuko bunifu wa ufadhili kwa elimu ya watoto wakimbizi

Mfuko mpya kwa ajili ya kufadhili huduma za elimu duniani kote utazinduliwa wakati wa Kongamano la kimataifa kuhusu masuala ya kibinadamu, WHS, linalofanyika mwezi huu mjini Istanbul, Uturuki.

Lengo ni kuhudumia watoto milioni 30 waliolazimika kuhama makwao.

Mfuko huo unaoitwa “Elimu haiwezi kusubiri”unatarajiwa kuungwa mkono na zaidi ya wadau 100, wakiwemo nchi, makampuni na watu binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini NEw York kwa njia ya simu, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya elimu Gordon Brown amesema hatua zinapaswa kuchukuliwa mara moja ili kudhibiti madhara yatokanayo kukosa elimu kwa kizazi kizima cha vijana na watoto.

Bwana Brown amesema zaidi ya dola bilioni 3.8 zitahitajika kwa kipindi cha miaka mitanoijayo, wakati ambapo takwimu za ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA zikionyesha kwamba asilimia 2 tu za fedha za misaada ya dharura zinalenga huduma za elimu.

(Sauti ya Brown)

“Mfuko huo utakuwa wa kipekee kwa njia mbalimbali. utakuwa ni ubia baina ya sekta za umma na sekta binasi. Tutakuwa na fursa maalum kwa kampuni za teknolojia za habari kwa sababu ya umuhimu wa elimu kupitia mitandao kwa watoto waliolazimika kuhama makwao ambao hawana fursa nyingine ya kusoma mbali na kutumia simu za mkononi na ipads.”