Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban apigia chepuo Mahakama ya ICJ inapoadhimisha miaka 70

Ban apigia chepuo Mahakama ya ICJ inapoadhimisha miaka 70

Ikiwa leo ni maadhimisho ya miaka 70 tangu kuasisiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa nchi zote zikubali mamlaka ya Mahakama hiyo, na kuheshimu uamuzi wake. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Ban amesema hayo akifungua sherehe za maadhimisho hayo ya miaka 70, ambapo amesema kuheshimu utawala wa sheria ndani na baina ya mataifa, ni moja ya misingi ya maendeleo katika kila sehemu ya kazi ya Umoja wa Mataifa.

Aidha, Ban amesema, utawala wa sheria ni kiungo muhimu katika Ajenda mpya ya 2030 ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Ban amesema, kwa miongo saba iliyopita, Mahakama ya Kimataifa ya Haki, kama chombo kikuu cha sheria cha Umoja wa Mataifa, imechangia kwa kiwango kikubwa kwa utawala wa sheria, na hivyo kuipigia chepuo

"Natoa wito kwa mataifa yote ambayo hayajakubali mamlaka ya Mahakama hii, kuyakubali, na pia natoa wito wa kutekeleza haraka uamuzi uliotolewa na Mahakama hii" 

Mahakama ya ICJ ina makao yake makuu Uholanzi, kwenye jumba la amani lililoko The Hague. Kama ilivyo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, Mahakama hii nayo ni chombo kikuu cha Umoja wa Mataifa.

Ni chombo pekee kati ya vile vya Umoja wa Mataifa kisicho na makao yake mjini New York. ICJ ni chombo kikuu cha kisheria cha Umoja wa Mataifa na ni Mahakama ya ngazi ya juu kabisa ya kimataifa. 

image
Mahakama imekuwepo tangu mwaka 1946. Kiingereza na Kifaransa ndizo lugha rasmi za utendaji. Nyaraka ya kuanzisha ICJ ni sehemu ya mkataba ulioanzisha Umoja wa Mataifa. Kwa mantiki hiyo, wanachama wote wa Umoja wa Mataifa wanatambua uwepo wa Mahakama hii na wanaweza kutumia huduma zake.

Mahakama ya kimataifa ya haki ina majukumu mawili:

Mosi ni kuamua mivutano baina ya mataifa. Hapa tunazungumzia kesi zinazoweza kuleta mvurugano.

Jukumu la pili la ICJ ni kujibu hoja za kisheria zinazowasilishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama na vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika yake. Hapa tunazungumzia mchakato wa ushauri

ICJ siyo Mahakama ya uhalifu: Haihukumu mtu mmoja mmoja. Ni mashauri ya mizozo tu baina ya nchi ndiyo yanawasilishwa kwa Mahakama hii.

Mahakama ina majaji 15 wanaochaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  na Baraza la usalama kwa kipindi cha miaka Tisa.

image
Majaji wa Mahakama ya ICJ (Picha: ICJ)
Nafasi Tano hubadilishwa kila baada ya miaka mitatu na majaji wanaweza kuchaguliwa zaidi ya mara moja.

Majaji lazima watoke nchi tofauti, lakini hawawakilishi nchi zao bali wanakuwa majaji huru.

Jopo la majaji linaakisi mgawanyo wa kijiografia ufuatao:

Viti vitatu vya majaji ni kutoka Afrika; Viti viwili ni majaji kutoka Amerika Latina na Karibea; Viti vitatu ni majaji kutoka Bara Asia; Majaji wengine watano wanatoka Ulaya Magharibi na nchi nyingine za Magharibi; na majaji wawili kutoka Ulaya Mashariki.

Hakuna nchi yenye haki ya kuwa na kiti cha jaji, lakini kiutekelezaji, Mahakama imekuwa kila wakati inajumuisha jaji mmoja kutoka kila nchi tano zenye ujumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.