Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ataka uungwaji mkono kwa mpango wa kupambana na ugaidi

Ban ataka uungwaji mkono kwa mpango wa kupambana na ugaidi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, leo ameomba nchi wanachama wa Umoja wa mataifa kuunga mkono mpango wake wa kupambana na ugaidi, wakati wa kongamano kuhusu kuzuia itikadi kali katili linaloendelea mjini Geneva Uswisi. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Bwana Ban amesisisitza kwamba ugaidi hauhusiani na dini, kabila au taifa moja tu, bali unaathiri dunia nzima. Hata hivyo ameongeza kwamba wengi wa wahanga ni Waislamu.

Katibu Mkuu amezingatia hatari ya tishio la ugaidi kwa mshikamano wa jamii, usalama wa kimataifa, na maadili ya Umoja wa mataifa.

Amefafanua zaidi mpango wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ugaidi, akieelezea kwamba cha msingi ni kuzuia vitendo hivyo visitokee kwa kukabiliana kwa pamoja na mizizi yake vikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa ajira na mivutano ya kisiasa.

(Sauti ya Bwana Ban)

"Kuzuia itikadi kali katili kunapitia njia mbalimbali, lakini dharura zaidi ni kutunza na kuwezesha wavulana na wasichana. Wao ni wahanga mara mbili: Wanashawishiwa kujiunga na vikundi kali katili na pia wanashambuliwa kwenye sehemu za burudani, shule na vyuo."