Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pengo la chakula linaongezeka Sudan Kusini:UM

Pengo la chakula linaongezeka Sudan Kusini:UM

Mgogoro na uhaba wa mvua vimepunguza zaidi uzalishaji wa chakula Sudan Kusini na kuchangia upungufu wa tani 381,000 za nafaka ikiwa ni asilimia 53 zaidi ya ilivyokuwa mwaka 2015 kwa mujibu wa ripoti ya tathimini ya shirika la chakula na kilimo FAO na lile la mpango wa chakula duniani WFP.Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Mashirika hayo yamesema mgogoro wa Sudan Kusini unaingiliana na kiwango cha kutisha cha njaa, watu milioni 5.8 au karibu nusu ya watu wote nchini humo hawana uhakika na wapi mlo wao wa baadaye utakapotokka huku kiwango cha upungufu wa usalama wa chakula sasa kikiwa kimefikia asilimia 12.

Mashirika hayo yameongeza kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na mchanganyiko wa vita vinavyokatili maisha ya watu, hali mbaya ya uchumi na mvua hafifu. Kwa pamoja matatizo yoye haya yanaongeza pengo la njaa ambalo yanahofia litawalazimisha watu zaidi kushinda njaa na ongezeko la utapiamlo.

Mashirika hayo yameweka wazi kwamba ili kuimarisha hali ya chakula kunahitajika suluhu ya amani ya mgogoro.