Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utapiamlo wapungua Rwanda, lakini kazi bado ipo

Utapiamlo wapungua Rwanda, lakini kazi bado ipo

Utafiti mpya uliotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP na Wizara ya Kilimo ya Rwanda umeonyesha kwamba kiwango cha utapiamlo kimepungua kwa kiasi kikubwa nchini Rwanda kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, lakini bado kiko juu hasa kwenye maeneo ya vijijini.

Kwa mujibu wa utafiti huo, uwiano wa watoto wenye umri wa chini wa miaka mitano waliodumaa umeshuka kutoka asilimia 43 mwaka 2013 hadi 36.7 mwaka 2015, tatizo hilo likikumba zaidi maeneo ya vjijini.

Mkuu wa WFP nchini Rwanda, amesema mwelekeo huo unaonyesha kwamba Rwanda imepiga hatua kubwa katika kupambana na utapiamlo, lakini bado juhudi zaidi zinahitajika.

Umaskini, ujinga wa kusoma na kuandika na ukosefu wa ardhi kwa ajili ya kilimo ni sababu zilizotajwa na WFP katika kueleza uwepo wa tatizo hilo.

WFP ambayo tayari inawapatia zaidi ya watu 200,000 nchini Rwanda misaada ya kijamii ikiwemo mlo wa shuleni imependekeza kubaini mikakati ya kitaifa itakayolenga watu maskini zaidi wanaoishi vijijini na kuwapatia misaada ya msingi ya kijamii hasa wakati wa mwambo.