Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madai ya ukatili na unyanyasaji wa kingono DRC, walinda amani wa Tanzania wazuiliwa

Madai ya ukatili na unyanyasaji wa kingono DRC, walinda amani wa Tanzania wazuiliwa

Walinda amani wa Tanzania wanaotuhumiwa na ukatili na unyanyasaji wa kingono huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wamezuiliwa kambini wakati uchunguzi dhidi ya tuhuma zao ukisubiriwa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani kuwa hatua hiyo inafuatia visa 11 vilivyowasilishwa mwishoni mwa wiki kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO.

Amesema visa vyote hivyo vinahusiana na madai ya matunzo ya watoto ambao yadaiwa baba zao ni walinda amani wa Tanzania walio kwenye kikosi cha kujibu mashambulizi cha MONUSCO, IFB.

(Sauti ya Dujarric)

“Visa vinne kati ya hivyo vinahusisha walinda amani katika kikosi cha sasa na vilivyosalia ni waliokwishaondoka. Kamanda wa kikosi cha Tanzania  anawashikilia kwenye kituo chao walinda amani wanaotuhimiwa wakisubiri uchunguzi zaidi. Halikadhalika askari wote wamezuiliwa kambini.”

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Ban Ki-moon pamoja na kupendekeza hatua dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyofanywa na walinda amani, alipendekeza nchi wanachama zipokee malalamiko kutoka kwa wahanga kuhusu usaidizi wa kifedha sambamba na kuunda kitengo kitakachofuatilia madai yanayohusu kusaka baba wa watoto.