Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama ndio ufunguo wa maendeleo ya nishati ya nyuklia- IAEA

Usalama ndio ufunguo wa maendeleo ya nishati ya nyuklia- IAEA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Yukiya Amano, amesema leo kuwa usalama ni suala muhimu kwa maendeleo ya nishati ya nyuklia katika siku zijazo.

Amano amesema hayo akihutubia mkutano wa 2016 kuhusu sekta ya nyuklia, ambao unamulika udhibiti wa vitisho vya kupitia kwenye mtandao wa intaneti, kudumisha usalama wa matumizi, hifadhi na usafirishaji wa bidhaa za minururisho na za nyuklia, pamoja na mchango wa sekta ya nyuklia duniani.

Bwana Amano amesema licha ya ajali ya nyuklia ya mtambo wa Fukushima Daiichi nchini Japan miaka mitano iliyopita, matumizi ya nishati ya nyuklia duniani yanatarajiwa kuendelea kukua, ingawa kwa kasi ndogo kuliko ilivyotabiriwa.

Ameongeza kwamba nchi nyingi zinaamini kuwa nishati ya nyuklia inaweza kuzidaidia kufikia malengo mawili ya kuongeza uzalishaji wa umeme na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, na kwamba kazi ya IAEA ni kuhakikisha kuwa zinapowekeza katika nishati hiyo, zinafanya hivyo kwa njia salama.

Kufikia sasa kuna mitambo 442 ya vinu vya nyuklia inayofanya kazi katika nchi 30, na mingine 66 inajengwa, hususan barani Asia.