Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miradi ya kibinadamu Syria yapigwa jeki kwa dola milioni 19

Miradi ya kibinadamu Syria yapigwa jeki kwa dola milioni 19

Takriban dola milioni 19 za Kimarekani zimetolewa kwa wadau wa kibinadamu nchini Syria kupitia mfuko wa pamoja wa kibinadamu, HPF.

Fedha hizo zitafadhili utoaji huduma za maji, kujisafi na usafi, lishe, afya, uhakika wa kuwa na chakula na kilimo, elimu, pamoja na miradi mingine ya sekta mseto, ili kukidhi mahitaji na kubadilisha maisha ya takriban watu milioni 1.4.

Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu nchini Syria, Yacoub El Hillo, amesema kuwa kufuatia kutengamaa kwa hali hivi karibuni, Umoja wa Mataifa na wadau wake wataongeza kasi ya jitihada zao kadri wanavyowezeshwa kuzifikia jamii ambazo hazijaweza kufikiwa na misaada kwa miezi kadhaa sasa.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 13.5 nchini Syria wanahitaji usaidizi wa kibinadamu mwaka huu 2016, wakiwemo watu milioni 4.6 walioko katika maeneo magumu kufikiwa, nusu milioni wakiwa wamezingirwa.