Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano mapya kati ya EU na Uturuki kuhusu wakimbizi huenda yakawaweka watoto hatarini: UNICEF

Makubaliano mapya kati ya EU na Uturuki kuhusu wakimbizi huenda yakawaweka watoto hatarini: UNICEF

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeelezea wasiwasi wake kwamba makubaliano mapya baina ya Muungano wa Ulaya na Uturuki ambayo yanaanza kutekelezwa wiki hii , hayashughulikii tatizo muhimu la mahitaji ya kibinadamu kwa watoto wakimbizi na wahamiaji 19,000 waliokwamba nchini Ugiriki.

Shirika hilo linasema watoto ni asilimia 40 ya wakimbizi na wahamiaji wote walioko Ugiriki. Na linakadiria kwamba watoto walio peke yao bila wazazi au walezi ni asilimia 10 ya watoto wote.

UNICEF imeonya kwamba makubaliano hayo mapya huenda yakawalazimu watoto na familia kuchukua njia mbadala ya hatari zaidi ikiwemo kuvuka bahari ya Mediteranea. Sarah Crowe ni msemaji wa UNICEF

(SAUTI YA SARAH CROWE)

"Watoto wasioambatana na mzazi  au mlezi wanapaswa kusajiliwa ipasavyo na kupelekwa kwenye vituo vya kuwalinda badala ya kufungwa. Hakuna mtoto anayepaswa kufungwa kwa msingi wa kuwa mkimbizi au mhamiaji.  Watoto wana haki ya kusikilizwa kabisa na hali yao kutathminiwa kabla ya uamuzi wowote kuwahusu, ikiwemo kurudhishwa."