Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kirusi cha Zika chapenyeza hadi kwa mtoto aliye tumboni- WHO

Kirusi cha Zika chapenyeza hadi kwa mtoto aliye tumboni- WHO

Mkutano wa pili wa kamati ya dharura ya shirika la afya ulimwenguni, WHO kuhusu kirusi cha Zika umehitimisha leo huko Geneva, Uswisi kwa kuelezwa kuwa mwelekeo wa sasa wa kirusi hicho unazidi kutia shaka.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema tafiti zinazoendelea zimebaini kuwa kirusi hicho sasa siyo tu kinasambazwa kupitia mbu bali pia kwa njia ya ngono.

Na zaidi ya hapo, tafiti zimebaini kirusi cha zika kwenye majimaji yaliyoko ndani ya nyumba ya uzazi anamokuwepo mtoto wakati wa ujauzito.

“Kuhusu uhusiano wa mtoto kuzaliwa na kasoro, ushahidi umeonyesha kuwa kirusi kinaweza kuvuka kingo za nyumba ya uzazi na kuingia kwa mtoto aliye tumboni. Tunaweza sasa kuhitimisha kuwa kirusi cha Zika kinaweza kuingia kwenye mishipa ya fahamu na kuharibu tishu kwenye ubongo wa mtoto ambaye hajazaliwa.”

Amesema kirusi pia kimebainika kwenye damu, tishu za ubongo na majimaji ya ubongo wa watoto ambao wamefia tumboni, ambao mimba ziliharibika au mimba zilizotolewa.

Kwa hiyo pendekezo la kamati hiyo ni kuendelea kusaka ushahidi juu ya uwezekano wa uhusiano kati ya maambukizi ya kirusi cha Zika na matatizo ya ubongo sanjari na kuendeleza kuimarisha hatua za umma kujikinga badala ya kusubiri majibu ya kisayansi.