Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon atembelea Goma, DRC

Ban Ki-moon atembelea Goma, DRC

Akiendelea na ziara yake Maziwa Makuu barani Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon baada ya kutoka Burundu ameelekea Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo amewasili asubuhi mashariki mwa nchi hiyo. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Katika uwanja wa ndege wa Goma Bwana Ban amelakiwa na mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo Maman Sidiku na Gavana wa Kivu Kaskazini Julien Paluku, ambao wamemsindikiza kutembelea kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kitchanga.

Kambi hiyo ni makazi ya wakimbizi wapatao 15,000 waliokimbia mapigano Kivu Kaskazin. Kambini humo Bwana Ban ametemebelea duka la kuoka na kuuza mikate, shule ya msingi na kukutana na kikundi cha wanawake.

Akizungumza na waandishi wa habari kambini Kitchanga, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa usaidizi wa kibinadamu kwa watu wanaoteseka zaidi

(Sauti ya Bwana Ban)

"Yote niliyoyasikia nimeyaona mwenyewe. Nimeguswa sana. Kama Katibu Mkuu, nataka kukutana na walioteseka zaidi. Nataka kuwa mtetezi wao; sauti ya wale waliokosa sauti. Nadhani tunapaswa kuimarisha usaidizi wa kibinadamu. Ndio maana naitisha kongamano la kwanza la kimataifa kuhusu maswala ya kibinadamu mjini Istanbul, mwezi Mei."

Baada ya kuzuru kambi ya Kitchanga, Katibu Mkuu amerejea Goma ambapo amekutana ana kwa ana na Daktari Denis Mukwege aliyeshinda tuzo ya kimataifa kwa juhudi zake katika kupambana na ukatili wa kingono DRC.

Baadaye leo Katibu Mkuu ataelekea Kinshasa ambapo kesho atakutana na Rais Joseph Kabila, viongozi wa jamii na vyama vya upinzani na pia kuhudhuria mkutano wa wawekezaji kwenye ukanda wa maziwa makuu.