Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya baada ya uchaguzi Uganda inatia wasiwasi:UM

Hali ya baada ya uchaguzi Uganda inatia wasiwasi:UM

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema inatiwa wasiwasi na hali baada ya uchaguzi nchini Uganda, huku kukiwa na taarifa za kuuwawa kwa watu wawili, idadi isiyojulikana ya majeruhi, na idadi kubwa ya polisi na jeshi kumiminwa mitaani Kampala na kutiwa mbaroni kwa viongozi wanne wa upinzani tangu siku ya uchaguzi.

Ofisi hiyo imesema Bwana  Kizza Besigye, kiongozi wa FDC (Forum for Democratic Change), amekamatwa na kuachiwa mara tatu juma lililopita na kuwekwa katika kifungo cha nyumbani Jumapili bila mashitaka yoyote . Jana Jumatatu asubuhi alipelekwa katika kituo cha polisi cha  Nagalaama, kilometa 30 kutoka mji mkuu  Kampala, alipojaribu kuondoka nyumbani kwake.

Imesema viongozi wengine ni wagombea wawili wa Urais Amama Mbabazi, wa chama cha Go Forward party, ambaye amekuwa katika kifungo cha nyumbani tangu Jumamosi, wakati  Abed Bwanika, Rais wa chama cha  PDP (People's Development Party),alikamatwa na polisi  Ijumaa eneo la Mutukula, karibu na mpaka wa Tanzania alipokua akijaribu kuondoka nchini na familia yake, naye mayor wa Kampala Erias Lukwago, alikamatwa  Jumamosi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukamatwa kwa Besigye.  Cecily Poully ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu anaongeza...

(SAUTI YA CECILY POULY)

"Tunasikitishwa  pia na matumizi ya nguvu  yaliyofanywa na polisi na jeshi siku ya Ijumaa kwa ajili ya kutisha na kuwafurusha watu kutoka makao makuu ya FDC jijini Kampala. Imeripotiwa mabomu ya kutoa machozi yalitumika pamoja na risasi. Halikadhalika taarifa za waandishi habari kuteswa na kutishiwa na vikosi vya usalama."